1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Qatar yasema mateka zaidi kuachiwa

28 Novemba 2023

Makubaliano ya kusimamisha vita kati ya Israel na Hamas yameingia siku ya tano Jumanne, huku wanamgambo wa Hamas wakitarajiwa kuwaachia huru mateka zaidi.

https://p.dw.com/p/4ZXYH
Baadhi ya mateka wa Israel waachiwa huru
Picha hii iliyotolewa na jeshi la Israel inaonesha mateka wa Israel Sahar Kalderon aliyeachiwa huru akikumbatiana na jamaa zake wakati alipowasili katika kituo cha matibabu cha Sourasky mjini Tel Aviv siku ya Jumatatu 27.11.2023 baada ya kushikwa mateka na wanamgambo wa Hamas katika Ukanda wa Gaza.Picha: AP/picture alliance

Pande hizo mbili zilikubaliana kurefusha muda wa kusitisha vita hadi kesho Jumatano huku kukiwa na mipango miwili ya kuwaachia mateka wanaoshikiliwa na Hamas na kwa upande wa Israel kuwaachia wafungwa wa Kipalestina walioko katika magereza ya Israel.

Hali hiyo inatizamwa kuwa mbinu ya Hamas kuchelewesha kurejea kwa vita vya Israel. Wakati huo huo shinikizo linaongezeka kwa Israel kuwaepusha raia wa Palestina dhidi ya mashambulizi wakati itakapoanza upya mashambulizi yake huko Gaza.

Qatar ambayo inahusika pakubwa na juhudi za upatanishi imesema lengo na matumaini ya wajumbe kwenye makubaliano kati ya Israel na Hamas kwa sasa ni kuendeleza kusimamishwa mapigano ili kuyapa nafasi mazungumzo zaidi.

Fahamu zaidi kuhusu mateka wa Israel chini ya Hamas

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar, Majed al-Ansari amesema kulingana na makubaliano inategemewa Hamas kuwaachilia mateka 10 kwa kila siku ya ziada ya usitishaji vita.

Makubaliano ya kuwaachia mateka wa Israel
Helikopta ambayo imewabeba mateka walioachiwa huru na Hamas ikiwasili katika hospitali ya Sourasky mjini Tel Aviv israel, Novemba 28, 2023.Picha: Athit Perawongmetha/REUTERS

Qatar: Usitishaji zaidi wa vita unategemea Hamas kuachia mateka

"Hadi sasa tuna uhakika kuwa mateka 20 wataachiliwa kati ya Jumanne na Jumatano. Bila shaka ndani ya saa 48, kutakuwa na juhudi za kurefusha muda zaidi wa usitishaji mapigano. Lakini hilo pia itategemea ikiwa Hamas wataachilia mateka zaidi," amesema al-Ansari.

Je Mzozo wa Israel na Hamas utaathiri vipi mkutano wa COP28?

Israel imeahidi mara kwa mara kuwa punde itakapokuwa dhahiri kuwa hakuna mateka zaidi watakaoachiliwa huru chini ya makubaliano ya sasa, itarejea vitani ili kuangamiza Hamas, kundi ambalo pamoja na nchi nyingine ikiwemo Marekani hulitaja kuwa la kigaidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekariri wito wake wa kusimamishwa vita kwa muda mrefu na kuachiliwa huru kwa mateka wote.

Olaf Scholz aahidi serikali yake yashinikiza kuachiwa kwa mateka wote

Naye kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameahidi kuwa serikali yake imejitolea kikamilifu kuhakikisha mateka zaidi wanaoshikiliwa na Hamas huko Ukanda wa Gaza wanaachiwa huru.

Kupitia taarifa ya serikali kwa bunge la Ujerumani siku ya Jumanne, Scholz ameelezea kuwa amefarijika juu ya kuachiwa baadhi ya mateka katika siku za hivi karibuni.

Vijana wawili wa Kijerumani ni miongoni mwa mateka walioachiwa huru hivi karibuni.
Vijana wawili wa Kijerumani ni miongoni mwa mateka walioachiwa huru hivi karibuni.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kutokana na kwamba Wajerumani ni miongoni mwa mateka walioachiliwa, Scholz amesema hiyo ni sababu nyingine ya kufurahia.

Usitishaji vita waibua matumaini ya mateka zaidi kuachiwa

Hamas pamoja na wanamgambo wengine wanawashikilia takriban mateka 160 kati ya 240 waliowakamata walipofanya shambulizi la kigaidi mnamo Oktoba 7 kusini mwa Israel na kuua takriban watu 1,200.

Antony Blinken kurudi Mashariki ya Kati

Katika tukio jingine, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, anatarajiwa kurudi tena Mashariki ya Kati mwishoni wiki hii kutafutia mzozo huo ufumbuzi zaidi.

Hiyo itakuwa mara ya tatu Blinken anafanya ziara hiyo tangu vita hivyo vilipoanza, na anatarajiwa kushinikiza kuendelezwa kwa usitishaji vita na kuachiwa huru kwa mateka zaidi.

Kulingana na takwimu za wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya Wapalestina ambao wameuawa kufuatia mashambulizi ya Israel tangu vita vianze imefikia 13, 300.

Utawala wa rais wa Marekani Joe Biden umeiambia Israel kwamba ni sharti iepushe uhamishaji mkubwa wa watu na maangamizi ya watu wengi miongoni mwao raia wa Palestina ikiwa itarudi vitani.

Mnamo Jumatatu, mateka 11 waliachiliwa huru na kufanya jumla ya mateka ambao wameachiliwa huru kufikia sasa kufika 51. Israel vilevile imewaachilia wafungwa 150 wa Palestina.

Bonyeza hapa upate makala zaidi kuhusu mzozo wa muda mrefu wa Mashariki ya Kati

Vyanzo: APAE, DPAE