1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leverkusen haishikiki katika Bundesliga

27 Novemba 2023

Bayer Leverkusen mwishoni mwa wiki walirudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga baada ya kupata ushindi wa 3-0 ugenini walipokuwa wakicheza na Werder Bremen.

https://p.dw.com/p/4ZUa4
Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga Werder Bremen v Bayer Leverkusen
Wachezaji wa Leverkusen wakisherehekea bao la Jeremie Frimpong (katikati)Picha: Fabian Bimmer/REUTERS

Kocha wa Leverkusen Xabi Alonso ambaye timu yake pamoja na Bayern Munich zikiwa ndizo timu mbili pekee ambazo hazijaonja kushindwa msimu huu katika Bundesliga anasema, kibarua bado ni kikubwa kwa vijana wake licha ya matokeo mazuri wanayoendelea kuyapata kuelekea mapumziko ya Krismasi na majira ya baridi ya Bundesliga.

"Kwa kweli tutahitajika kujituma mno kwasababu tuna mechi nyingi katika wiki chache tu, ila tunajua kinachohitajika na bila shaka tutakuwa tayari. Wacha tu tuone jinsi mambo yatakavyokwenda," alisema Alonso.

Naye mchezaji wa kiungo cha kati wa Leverkusen Florian Wirtz ambaye amekuwa mmoja wa nyota wa timu hiyo msimu huu, hapa anaeleza kilichowapelekea kupata ushindi wa mabao matatu ugenini dhidi ya Bremen.

"Ingawa tulikwenda mapumzikoni tukiwa na uongozi wa 2-0, sifikiri kama tuliridhika na mambo yalivyokuwa. Tuliendelea kupambania malengo yetu na kazi tukaifanya mpaka mwisho," alisema Wirtz.

Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga Werder Bremen v Bayer Leverkusen | Florian Wirtz
Kiungo wa Leverkusen Florian WirtzPicha: Fabian Bimmer/REUTERS

Baada ya mechi 12 Leverkusen sasa wanaliongoza jedwali la Bundesliga wakiwa na pointi 34 na wanaowafuata ni Bayern Munich walio na jumla ya pointi 32.

Vyanzo: AP/Reuters