1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Tuongeze juhudi kukabili mabadiliko ya tabia nchi

28 Novemba 2023

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuondokana na kile alichokitaja kama "mzunguko wa hatari " kimataifa wa kuongezeka kwa joto na kuyeyuka kwa barafu.

https://p.dw.com/p/4ZWpH
Mabadiliko ya Tabianchi | Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na viongozi wa mataifa yalioendelea kuhusu mazingira.Picha: Tobias Schwarz/AFP/Getty Images

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, kabla ya mkutano huo, Guterres ameonya kwamba barafu ya bahari inayoyeyuka kwa kasi katika bara la Antaktika inachangia kuongezeka kwa viwango vya bahari.

Guterres ambaye amekuwa ziarani katika bara hilo anasema barafu huakisi miale ya jua, na kadri inavyotoweka, joto zaidi hufyonzwa kwenye angahewa ya dunia.

Hiyo ina maana viwango vya joto vitaongezeka, dhoruba zaidi, mafuriko, moto na ukame kote ulimwenguni.

Aidha katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amewatolea wito viongozi kuchukua hatua katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Soma pia:Guterres: Dunia inakabiliwa na mzozo wa mabadiliko ya tabianchi

Gutteres amesema viongozi lazima wachukue hatua kupunguza viwango vya joto duniani hadi nyuzi joto 1.5, kulinda watu kutokana na machafuko ya hali ya hewa, na kumaliza umri wa nishati ya mafuta.

Kunahitajika dhamira ya kimataifa ya kurejesha ufanisi wa nishati maradufu, na kuleta nishati safi kwa wote ifikapo 2030.

Katika Mkutano wa kilele wa COP28

Katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, utakaoanza kesho Alhamisi huko Dubai, zaidi ya nchi 190 zinataka kuchukua hatua katika utekelezaji wa Makubaliano ya Hali ya Hewa ya Paris ya 2015 kwa mara ya kwanza.

Mwanamke akitembea kwenye bango la tangazo la mkutano wa COP28
Mwanamke akitembea kwenye bango la tangazo la mkutano wa COP28 Picha: Sascha Schuermann/Getty Images

Huku haya yakijiri, mwenyeji wa mkutano huo Umoja wa Falme za Kiarabu, anapanga kuitumia "fursa" ya mikutano huo kufanya mikutano na wawakilishi wa serikali za kigeni kuzishawishi kushiriki katika mikataba ya mafuta.

Haya ni kwa mujibu wa nyaraka zilizopatikana na BBC.

Soma pia:Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa: Ni yepi matarajio ya mkutano wa mwaka huu

Nyaraka hizo zilionyesha kwamba Umoja wa Falme za kiarabu umetayarisha mazungumzo na nchi 20, ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza na Ujerumani, kuhusu fursa za kibiashara kwa kampuni ya nishati mbadala ya serikali ya Masdar.

Hata hivyo rais wa COP28Sultan Ahmed Al Jaber ambaye pia Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Abu Dhabi na Masdar na msemaji wa mkutano huo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba nyaraka zilizotajwa na BBC "sio sahihi na hazikutumiwa kwa COP28.

Ujerumani yaahidi euro bilioni mbili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi